Isaiah 29

Ole Wa Mji Wa Daudi


1 aOle wako, wewe Arieli, Arieli,
mji alimokaa Daudi!
Ongezeni mwaka kwa mwaka,
na mzunguko wa sikukuu zenu uendelee.

2 bHata hivyo nitauzunguka Arieli kwa jeshi,
utalia na kuomboleza,
utakuwa kwangu kama mahali
pa kuwashia moto madhabahuni.

3 cNitapiga kambi pande zote dhidi yako,
nitakuzunguka kwa minara
na kupanga mazingirwa yangu dhidi yako.

4 dUtakaposhushwa, utanena kutoka ardhini,
utamumunya maneno yako kutoka mavumbini.
Sauti yako itatoka katika nchi kama vile ya mzimu,
utanong’ona maneno yako toka mavumbini.


5 eLakini adui zako wengi watakuwa kama vumbi laini,
kundi la wakatili watakuwa
kama makapi yapeperushwayo.
Naam, ghafula, mara moja,

6 f Bwana Mwenye Nguvu Zote atakuja
na ngurumo, tetemeko la ardhi, na kwa sauti kuu,
atakuja na dhoruba, tufani na miali ya moto iteketezayo.

7 gKisha makundi ya mataifa yote yale yapiganayo dhidi ya Arieli,
yale yanayomshambulia yeye na ngome zake, na kumzunguka kwa jeshi,
watakuwa kama ilivyo ndoto,
kama maono wakati wa usiku:

8 hkama vile mtu aliye na njaa aotavyo kuwa anakula,
lakini huamka, bado njaa yake ingalipo,
kama vile mtu mwenye kiu aotavyo kuwa anakunywa maji,
lakini huamka akiwa anazimia, akiwa bado angali ana kiu.
Hivyo ndivyo itakavyokuwa kwa makundi yote ya mataifa
yanayopigana dhidi ya Mlima Sayuni.


9 iDuwaeni na kushangaa,
jifanyeni vipofu wenyewe na msione,
leweni, lakini si kwa mvinyo,
pepesukeni lakini si kwa kileo.

10 j Bwana amewaleteeni usingizi mzito:
Ameziba macho yenu (ninyi manabii);
amefunika vichwa vyenu (ninyi waonaji).

11 kKwa maana kwenu ninyi, maono haya yote si kitu ila maneno yaliyotiwa lakiri katika kitabu. Kama mkimpa mtu yeyote awezaye kusoma kitabu hiki, nanyi mkamwambia, “Tafadhali kisome,” yeye atajibu, “Mimi siwezi, kwa kuwa kimetiwa lakiri.” 12Au kama mkimpa mtu yeyote kitabu hiki asiyeweza kusoma na kumwambia, “Tafadhali kisome,” atajibu, “Mimi sijui kusoma.”

13 lBwana anasema: “Watu hawa hunikaribia kwa vinywa vyao
na kuniheshimu kwa midomo yao,
lakini mioyo yao iko mbali nami.
Ibada yao kwangu inatokana na maagizo
waliyofundishwa na wanadamu.

14 mKwa hiyo mara nyingine tena nitawashangaza watu hawa,
kwa ajabu juu ya ajabu.
Hekima ya wenye hekima itapotea,
nayo akili ya wenye akili itatoweka.”

15 nOle kwa wale wanaokwenda kwenye vilindi virefu
kumficha Bwana mipango yao,
wafanyao kazi zao gizani na kufikiri,
“Ni nani anayetuona? Ni nani atakayejua?”

16 oMnapindua mambo juu chini,
kana kwamba mfinyanzi aweza kufikiriwa kuwa kama udongo wa mfinyanzi!
Je, kile kilichofinyangwa chaweza kumwambia yule aliyekifinyanga,
“Wewe hukunifinyanga mimi?”
Je, chungu kinaweza kumwambia mfinyanzi,
“Wewe hujui chochote?”


17 pKwa muda mfupi sana, je, Lebanoni haitageuzwa kuwa shamba lenye rutuba,
na shamba lenye rutuba liwe kama msitu?

18 qKatika siku ile viziwi watasikia maneno ya kitabu,
na katika utusitusi na giza
macho ya kipofu yataona.

19 rMara nyingine tena wanyenyekevu watafurahi katika Bwana,
wahitaji watafurahi katika yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.

20 sWakatili watatoweka na wenye kudhihaki watatokomea,
nao wote wenye jicho la uovu watakatiliwa mbali,

21 twale ambao kwa neno humfanya mtu kuwa mwenye hatia,
wamtegeao mtego mtetezi katika mahakama,
na kwa ushuhuda wa uongo humnyima haki
yeye asiye na hatia.

22 uKwa hiyo hili ndilo Bwana, aliyemkomboa Ibrahimu, analosema kwa nyumba ya Yakobo: “Yakobo hataaibishwa tena,
wala nyuso zao hazitabadilika sura tena.

23 vWakati watakapoona watoto wao miongoni mwao,
kazi ya mikono yangu,
watalitakasa Jina langu takatifu;
wataukubali utakatifu wa yeye Aliye Mtakatifu wa Yakobo,
nao watamcha Mungu wa Israeli.

24 wWale wanaopotoka rohoni watapata ufahamu,
nao wale wanaolalamika watayakubali mafundisho.”
Copyright information for SwhKC